Ushirika Watakiwa Kujiendesha Kisasa na Kugusa Makundi Yote.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Dkt.Benson Ndiege, amevitaka vyama vya ushirika nchini, kujiendesha kisasa ikiwa ni pamoja na kuwa na ushirika wenye kugusa makundi yote, vijana, wazee, kina mama na wafanyakazi wa makundi yote.
Dkt. Ndiege amesema Tume imedhamiria kuimarisha zaidi matumizi ya Mifumo ya Kieletroniki katika ukusanyaji wa taarifa mbalimbali ambazo zitasaidia Ushirika kujiendesha kisasa.
Mrajis ameyasema hayo leo Septemba 10, 2021, jijini Dodoma wakati wa Kikao kazi cha wadau wa ushirika kutoka mikoa mbalimbali nchini wakati wa mapitio ya Mpango Mkakati wa Tume, ambapo amesema kwa sasa ni lazima kuwe na Ushirika wa kisasa na kuachana na uendeshaji wa Ushirika kwa mazoea.
“Lazima tubadilike tuwe na ushirika ambao unawagusa vijana,wazee kina mama na wafanyakazi na makundi yote; wavuvi, Waandishi wa Habari, lazima tusibaki na ushirika wa kizamani hata mifumo yetu lazima iende kisasa. Wewe kama unaendelea kutembelea na makaratasi wenzako wapo kwenye simu wanapata information lazima na sisi tuendane na hali halisi ya nchi yetu jinsi ilivyo,”amesema Dkt. Ndiege
Aidha, Dkt. Ndiege amesema ili Ushirika uweze kwenda vizuri ni lazima kuwe na imani kwa kile ambacho kinafanyika ambapo watu wasipokuwa na imani ni sawa na kazi bure.
“Kwa sasa tunachotamani kwa ukubwa ni imani katika vyama vya ushirika watu wasipokuwa na imani hata tupige kelele au tuweke mifumo gani hawatatumia fursa hizo.Unaweza ukaenda kijijini ukapiga shule yako wanakusikiliza wanakwambia miaka kumi chama chetu kilikuwa kinaleta pembejeo lakini sasa hivi hakuna.
“Hatuwezi kwenda bila kuleta imani hili ni jukumu letu sote lazima tuanze kwa kujenga imani kwa kuwa waaminifu,”amesema.Dkt.Ndiege
Amesema malengo yao ni kuhakikisha kunakuwa na vyama imara vya ushirika ikiwemo kuviona vyama hivyo vinakuwa na mifuko ya pembejeo ili viweze kujitegemea.
“Ni bora kuwa na vyama vichache na sisi tunajikita na kuwa na vyama imara vya ushirika kwa sababu hiyo tunayo malengo ambayo yatasaidia vyama, mojawapo kwenye vyama vya mazao tungependa kuona vyama hivyo vinakuwa na mifuko ya pembejeo na sisi tutajenga mazingira ili jambo hili liende vizuri,” amesema Dkt. Ndiege
“Tumejikita zaidi kuingia katika mifumo ya kieletroniki katika vyama vya ushirika na tayari zoezi hili limeanza na tutatunza taarifa vizuri na tunawaalika wadau kulifanikisha hili. Tunataka mifumo ioneshe wameingia wanachama wangapi na wamepata pembejeo kiasi gani,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Theresia Chitumbi amesema Mkutano huo upo kwa ajili ya kuaandaa ushirika mpya ambao utaenda kisasa.
“Tupo hapa kuaandaa mikakati ya Tume ya Ushirika kwani ni wadau wa ushirika tupo kwa ajili ya kuleta ushirika mpya na hilo ndio lengo la Rais wetu na tumeona nchi nyingi ambazo ushirika umesimama ndio wana maendeleo makubwa,”amesema
Amesema Ushirika wa zamani ulikuwa wa mazao tu lakini sasa hivi wamejipanga kuwavuta vijana na kuubadilisha ushirika na uwe wa kidigitali.
“Mimi kwa mtazamo wangu tunatakiwa kubadilika tuwe na ushirika wa kidigitali kuliko kwenye makatarasi ukiwa kidigitali kila kitu kinaonekana tumeanza kuwaingiza vijana,”amesema.