Wito Watolewa Ushirika Kuongeza Kasi Ya Viwanda
Vyama vya Ushirika vimetakiwa kuendeleza viwanda vinavyochakata bidhaa zinazozalishwa na Vyama hivyo kwa kuongeza thamani ya mazao yake ili kuweza kuendana na soko la ushindani la ndani na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa Septemba 01, 2021 na Waziri wa Kilimo, Mhe. Prof. Aldolf Mkenda, wakati akifungua Kongamano la Pili la Kimataifa la Ushirika katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).
Kongamano hilo limefanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba 01 - 03,2021 na limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC). Kauli mbiu ya Kongamano hilo ni Ushirika na Maendeleo ya Viwanda kwa kuzingatia maslahi ya wanachama.
Waziri ameeleza kuwa ni dhamira ya Serikali kuona Vyama vya Ushirika vinaongeza tija kwa kuongeza viwango vya uzalishaji ili iwe ni msukumo wa kuanzisha na kuendeleza Uchumi wa Viwanda kwa kuongeza thamani ya mazao na bidhaa zinazotokana na Vyama hivyo.
“Lengo la Serikali ni kuimarisha na kuendeleza Ushirika ingawa ushirika unakabiliwa na changamoto za Kisera, masuala ya Sheria, na hitaji la wataalamu katika utendaji wa Vyama vya Ushirika,” alisema Prof. Mkenda.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege amesema Tume kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013 itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuvisimamia vyma na kuhamasisha maendeleo yake.
“Ni wakati sasa Vyama vya Ushirika vifikirie kuwa na viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali na kuyaongezea thamani ili kuzalisha bidhaa zinazotokana na maziwa, asali, alizeti na mengine mengi,” alieleza Mrajis
Mrajis ameongeza kuwa hivi sasa Sekta ya Ushirika ina viwanda 452 ambavyo vinafanya shughuli mbalimbali za uchakataji na juhudi zinazoendelea katika kuendeleza na kuimarisha viwanda vya Ushirika ikiwemo uanzishaji wa Kiwanda cha vifungashio katika Chama Kikuu cha Ushirika SONAMCU mkoani Ruvuma, kiwanda cha kubangua Korosho cha Chama Kikuu cha Ushirika TANECU mkoani Mtwara, na kiwanda cha kuchambua Pamba cha Chama Kikuu cha Ushirika KACU mkoani Shinyanga.
Akichangia mada wakati wa Kongamano hilo, Mtaalamu wa Uchumi, Prof. Honest Ngowi ameshauri Vyama vya Ushirika vingi kwa sasa vinazalisha bidhaa na mazao yakiwa ghafi jambo ambalo bado linafanya tija na uchumi wa vyama hivyo kuwa duni.
Prof. Ngowi amesema kuwa uuzaji na usafirishaji wa mazao yaliyoongezwa thamani nje ya nchi unachangia kuongeza pato la Taifa, fursa za ajira, na uchumi wa mtu mmoja mmoja ambao hatimaye utachangia kupunguza umaskini. Akibainisha kuwa hadi kufikia 2020 viwanda vinachangia ajira kwa kiasi cha asilimia 40. Jambo ambalo likiimarishwa litainua uchumi hasa wa Sekta binafsi na hatimaye Taifa kwa ujumla.
Aidha, Mtaalamu huyo wa uchumi ameeleza kuwa wigo mpana wa vyama vya Ushirika kushiriki katika uchumi na maendeleo ya viwanda kutokana na dhana ya ushirika kuwa yenye uwezo wa kushirikisha Nyanja mbalimbali za uchumi ikiwemo vyama vya ushirika wa kilimo, uvuvi na maeneo mengine.
Shughuli nyingine zilizofanyika kwenye uzinduzi wa Kongamano hilo ni pamoja na utiaji saini wa mikataba ya Ushirikiano baina ya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, MoCU na Bodi ya Kahawa, MoCU na Shirikisho la Vyama vya Akiba na Mikopo nchini (SCCULT).
Mada zilizojadiliwa katika Kongamano hilo ni pamoja na masuala yanayohusu namna bora ya kuongeza uweledi katika utendaji wa vyama, Hifadhi ya Jamii kwa wanaushirika, mabadiliko na maboresho ya Sheria za Ushirika, Ushirikishwaji wa Vijana katika Vyama vya Ushirika. Mada hizi zililenga kujadili changamoto ili kupata mapendekezo ya suluhu za kuboresha Sekta ya Ushirika.