Chama Kikuu cha Ushirika cha Milambo kilichosajiliwa tarehe 18 Juni, 2018 kimepongezwa kutokana na mafanikio yaliyopatikana tangu kianzishwe kutokana na ubunifu katika kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa vyama vya msingi havitegemei mikopo kutoka benki kwa ajili ya pembejeo za kilimo.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Titus Kamani, jana Jumatano, Desemba 18, 2019 wilayani Urambo, alipokua kwenye ziara ya kutembelea vyama vya ushirika katika mkoa wa Tabora ambapo alipongeza juhudi zinazofanywa na viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Milambo katika kumuinua mkulima.
“Nawapongeza kwa kuhakikisha kuwa vyama vya msingi havitegemei mikopo kutoka benki kwa ajili ya pembejeo na msirudi nyuma katika kutekeleza mikakati yenu ya kuwainua wanaushirika ambao wamewakabidhi chama chao mkisimamie na kukiendesha kwa ufanisi mkubwa,” amesema Dkt. Kamani.
Dkt. Kamani amewahakikishia Wanaushirika kote nchini kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kusimamia na kuhakisha kuwa vyama vya ushirika vinakuwa imara na mali zote za vyama hivi zilizoibiwa na wajanja wachache zinarejeshwa na waliohusika kuwaibia wanaushirika wanafikishwa kwenye vyombo vya dola.
“Viongozi wa Vyama vya Ushirika endeleeni kuchapa kazi kwa kuzingatia weledi na uadilifu, jiepusheni na vitendo vya wizi wa mali za Wanaushirika na mjiepushe na vitendo vya rushwa,” amesema Dkt. Kamani.
Aidha, Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika amewataka Viongozi wa Vyama vya Ushirika kuweka kumbukumbu sahihi za mali za ushirika na kuweka wazi mali zote zinazomilikiwa na chama kwa wanachama wao ili kudumisha Utawala Bora katika kuongoza na kusimamia vyama hivyo.
Akiwasilisha Taarifa ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Milambo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Kaimu Meneja Mkuu wa chama hicho, James Mgaya amesema kuwa chama kimeweka mikakati mbalimbali ikiwemo: Ujenzi wa kiwanda cha kuchakata tumbaku na kutengeneza sigara na Ufufuaji wa vyama sinzia.
“Kwa kushirikiana na vyama vikuu vya tumbaku chini ya mradi wa pamoja wa wakulima tumbaku tumeridhia kujenga kiwanda cha kuchakata tumbaku na kutengeneza sigara katika wilaya ya Urambo. Hii itaongeza thamani ya zao la tumbaku na pia itaongeza uzalishaji kwa vyama vyetu na kuendana na sera ya serikali ya uchumi wa viwanda” alisema Mgaya.
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Kamani jana vilevile alitembelea Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU LTD – 2018 na baadhi ya vyama wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Milambo: Usindi na Itundu AMCOS ambapo alijionea maendeleo na changamoto za uendeshaji katika vyama hivyo. Leo asubuhi, Dkt. Kamani atafanya mkutano na Wadau wa Ushirika katika mkoa wa Tabora na badaye kuendelea kutembelea Vyama vya Ushirika katika Manispaa ya Tabora.