Elimu ya Ushirika Iwafikie Wanachama Wote- Naibu Mrajis
Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Nchini, Collins Nyakunga ametoa wito kwa Vyama vya Ushirika kuhakikisha kuwa vinatoa elimu ya Ushirika kwa Wanachama wao kwa Mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya Mwaka 2013.
Wito huo umetolewa wakati akifungua mafunzo kwa Wajumbe wa Bodi mbalimbali za Vyama vya Ushirika wanachama na Wadau wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika nchini (TFC) leo Alhamisi Desemba 10, 2020 Jijini Dodoma.
Naibu Mrajis amesema ni muhimu elimu ya Ushirika kuwafikia Wanachama wa Vyama vya Ushirika ili kuwawezesha kuwa na uelewa mpana wa masuala yanayofanyika katika Vyama vyao. Hivyo amewataka viongozi wa Ushirika waliokuwa katika mafunzo hayo kuhakikisha mambo muhimu watakayojifunza katika mafunzo hayo wanayafikisha kwa wanachama wao.
“Viongozi mna wajibu wa kuwaandaa wengine kuwa Viongozi kwa kuhakikisha kuwa Wanachama wenu wanapata elimu ya Ushirika; elimu ya Ushirika si ya viongozi tu bali ni kwaajili ya Wanachama wote kwakuwa hii ni haki yao ya Msingi ya Kiushirika,” alisisitiza Naibu Mrajis
Aidha, Bw. Nyakunga ametumia fursa hiyo kuwakumbusha Viongozi wa Ushirika kuendelea kutenga Fedha kutoka kwenye mapato ya ndani ya Vyama kwaajili ya kutoa elimu kwa Wanachama, Wajumbe wa Bodi, Viongozi na Watendaji kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika.
Baadhi ya Masuala muhimu yaliyoko katika mafunzo hayo ni pamoja na kuzingatia Sheria ya Vyama vya Ushirika, Dhana ya Ushirika, Utawala Bora, Wajibu wa Viongozi wa Vyama vya Ushirika, elimu ya Biashara, masuala ya Rushwa pamoja na mengine yatakayoongeza tija na ufanisi kwenye Vyama.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Shirikisho, Theresia Chitumbi amesema Mafunzo hayo yamelenga kuongeza uelewa wa Ushirika kwa Wanaushirika na ametoa rai kwa Vyama vya Ushirika kuendelea kujiunga na Shirikisho hilo ili kuwa na Sauti ya pamoja katika Vyama vya Ushirika.
Akieleza mikakati inayoendelea kutekelezwa na Shirikisho hilo Chitumbi ameeleza kuwa Shirikisho liko katika jitihada za kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha na kuendeleza Sekta ya Viwanda. Ambapo Shirikisho lipo katika hatua za awali za mikakati ya kuanzisha Kiwanda cha Vifungashio vya Magunia pamoja na Kiwanda cha Mbolea.
Mwenyekiti wa TFC amesema kuwa Mafunzo hayo yatafuatiwa na Mkutano Mkuu wa 25 wa Shirikisho hilo utakaofanyika kesho Ijumaa, Desemba 11, 2020 Jijini Dodoma. Mkutano huo utakaojumuisha Wajumbe, Viongozi, Wanachama na Wadau mbalimbali wa Ushirika kwaajili ya kujadili masuala na taarifa mbalimbali za Shirikisho hilo ili kupanga mikakati na mipango ya mbele ya Shirikisho hilo.