Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe, amesema kuwa Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa Mkulima wa Kahawa anapata bei nzuri itakayomnufaisha kupitia mfumo wa Ushirika. Bei ambayo itakuwa ni juu ya bei ya mauzo ya Kahawa ya mwaka jana ya Shillingi 2,260.
Naibu Waziri Bashe amesema hayo leo Jumatatu Mei 11, 2020 Jijini Dodoma wakati akiongoza kikao cha Wadau wa zao la Kahawa wa Mkoani Kagera; wakiwemo viongozi Vyama Vikuu vya Ushirika Kagera vya KDCU na KCU.
Mhe. Bashe amewataka viongozi wa Vyama vya Ushirika, watendaji na wadau wa zao hilo kushirikiana kwa pamoja na Serikali ili kuhakikisha kuwa ununuzi wa Kahawa msimu huu unakuwa wa ufanisi zaidi kupitia mfumo wa Ushirika kwa kumpatia mkulima bei nzuri itakayomnufaisha.
Naibu Waziri Bashe amewataka Wanunuzi wa Kahawa kufuata taratibu husika za Ushirika wakati wa ununuzi, ikiwemo uwazi na wenye ushindani na ameelekeza kuwa Bodi ya Kahawa iendelee kutoa miongozo husika ya ununuzi kwa wafanyabiashara na wanunuzi wa zao hilo nchini.
“Ni lazima tuangalie namna ambavyo mkulima atanufaika na kupata faida na kahawa yake, ushirika umpatie mkulima thamani ya zao hilo, tupitie kwa pamoja gharama za uendeshaji katika vyama vyetu vya Ushirika ili msimu huu mkulima apate bei nzuri,” alisema Naibu Waziri Bashe.
Aidha, Naibu Waziri ametoa ameitaka Benki ya Kilimo (TADB) kuendelea kutoa ushirikiano kwa Vyama vya Ushirika hasa katika utoaji wa mikopo na ununuzi wa zao hilo kwa kuzingatia kushusha riba ya mikopo kwa vyama hivyo kwa lengo la kumpa nafuu ya gharama za uendeshaji mkulima. Sambamba na hilo Mhe. Bashe amevitaka Vyama Vikuu kutathmini namna bora ya kupunguza gharama za uendeshaji ili kupunguza gharama hizo kwa mkulima.
Matumizi ya Akaunti za Benki kwa Wakulima ni moja ya suala lililosisitizwa katika majadiliano ya kikao hicho, ambapo Mhe. Bashe amewataka viongozi wa Vyama Vikuu kufuatilia kwa karibu suala la Wakulima katika Vyama vya Msingi (AMCOS) na kuhakikisha kuwa Wakulima wanakuwa na Akaunti za Benki kwaajili ya kuhakikisha wanapata malipo yao kwa usahihi na kupunguza udanganyifu na ubadhilifu kwa wakulima.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Bashe ameagiza wale wote waliohusika kuingiza hasara Vyama Vikuu vya KDCU na KCU ya Shillingi Bilioni saba (7) watafutwe, uchunguzi ufanyike na watakaobainika hatua madhubuti zitachukuliwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu.
Akiongea katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera, Rashid Mwaimu amesema kuwa elimu ya Ushirika bado ni ndogo kwa wakulima na Wanaushirika ambapo ameshauri kuongezeka kwa matumizi ya Vyombo vya Habari ili kuwafikishia wakulima taarifa sahihi.