Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa wakulima wa mazao mbalimbali nchini kuongeza matumizi ya Mfumo wa Ushirika kwa kutumia Stakabadhi za Ghala ili kupata uhakika wa masoko na bei zenye tija kwa wakulima.
Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa akizindua Maadhimisho ya Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima NaneNane, Kitaifa leo Agosti 01, 2020 katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.
Makamu wa Rais amesema kuwa ni muhimu wakulima kuuza mazao yao kupitia vyama vya Ushirika nchini hususan maeneo ambayo tayari yana mifumo imara ya Stakabadhi za Ghala. Aidha, ametoa wito kwa mikoa yote kujiandaa vyema na matumizi ya mifumo ya Ushirika na Stakabadhi za Ghala ili kupata bei zenye tija na zenye manufaa kwa wakulima.
“Tumeimarisha masoko ya mazao ya kilimo kupitia mfumo wa Stakabadhi za Ghalani. Serikali imeimarisha mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa kuhakikisha mazao yanauzwa kwa mfumo huo kupitia vyama vya ushirika ili kuwapatia wakulima masoko ya uhakika na bei zenye tija,” alisisitiza Makamu wa Rais
Akizungumzia kuhusu kauli mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu 2020, isemayo “Kwa maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua viongozi Bora 2020”, Mama Samia amesema kuwa inaendana na kipindi hiki ambacho tunaelekea Uchaguzi Mkuu wa Viongozi mbalimbali nchini. Hivyo wananchi watumie fursa hiyo kuchagua viongozi bora watakaoleta mapinduzi chanya katika Sekta za Uchumi wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
“Wakati wa uchaguzi utakapofika tumieni fursa hiyo kuchagua viongozi watakaoleta mapinduzi chanya kwa kusimamia Sera, uhakika wa masoko na maslahi mapana ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na maendeleo ya Taifa,” alisema Mhe. Samia.
Katika uzinduzi huo Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga, alitaja baadhi ya maeneo ambayo Serikali imeendelea kuweka msukumo wa maendeleo ya kimkakati ni pamoja na usajili wa wakulima kwaajili ya upatikanaji wa takwimu sahihi, kujua maeneo ya wakulima, mahitaji yao kwaajili ya kuongeza ufanisi wa uzalishaji wa mazao. Sambamba na hilo Mheshimiwa Hasunga amesema kuwa Serikali inafanya mapitio ya Sera ya Kilimo ya mwaka 2003 kwa lengo la kuanzisha Sheria ya Kilimo, uzinduzi wa Bima ya mazao, uimarishaji wa masoko ya mazao ya kilimo, uimarishaji wa mifumo ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo sahihi kwa wakati.