TAARIFA KWA WAANDISHI WA HABARI
MWONGOZO WA BIASHARA KWA KUTUMIA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA WA MWAKA 2021 KWENYE MAZAO YA CHOROKO, SOYA, UFUTA, MBAAZI NA DENGU
Ndugu Waandishi wa Habari, Serikali imekuwa ikihimiza matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwenye mazao na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na waweka mali (wakulima) na kuuzwa kwa kutumika mfumo huu rasmi wa biashara kwa lengo la kuleta tija kwa mauzo ya mazao na bidhaa ili kukuza kipato cha mkulima.
Ndugu Waandishi wa Habari, Katika kutekeleza adhma hii ya Serikali, Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kwa kushirikiana na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) imeandaa Mwongozo wa biashara kwa kutumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala wa Mwaka 2021 kwenye mazao ya Choroko, Soya, Ufuta, Mbaazi na Dengu kwa lengo la kuhamasisha uzalishaji wenye tija na kupata bei zenye ushindani.
Ndugu Waandishi wa Habari, Mwongozo huu unatoa maelekezo kuwa mazao haya yatakusanya kwenye ghala za vyama vya Ushirika na kusafirishwa kwenda kwenye ghala kuu (ghala za mnada) ambapo taarifa za mazao yaliyopokelea ghala kuu zitatumwa Soko la Bidhaa na kuuzwa kwa minada kwa njia ya kielektroniki. Hivyo basi niwaombe viongozi wote katika ngazi za mikoa na wilaya ambapo mazao haya yanalimwa, kusimamia utekelezwaji wa mwongozo huu.
Ndugu Waandishi wa Habari, Mwongozo huu unaelekeza kwamba malipo ya fedha za mauzo yatafanyika ndani ya siku tano za kazi kwa wakulima na wadau wengine baada mnunuzi kulipa. Malipo haya yanafanywa na mnunuzi kwenye Akaunti ya Soko la Bidhaa Tanzania na fedha zitahamishwa kwenda Akaunti ya Chama kikuu cha Ushirika ndani ya masaa 12.
Ndugu Waandishi wa Habari, Mwongozo huu unaelekeza kuwa kila mkulima na wadau wengine watalipwa fedha zao zote kupitia akaunti benki. Hivyo, ili kurahisisha malipo haya kufanyika kwa wakati, kila mkulima anatakiwa kuwa na akaunti yake. Mfumo huu wa malipo kupitia akaunti benki ni salama kwa wakulima wetu na unaleta usalama wa fedha yenyewe kwa mkulima.
Ndugu Waandishi wa Habari, kwa mujibu wa mwongozo huu, kila mnunuzi ambaye anahitaji kununua mazao haya anatakiwa kuanzia sasa kwenda kujisajili Soko la Bidhaa Tanzania ili aweze kushiriki katika minada ambayo itakuwa inafanyika kila wiki. Usajili huu unafanyika kwa njia ya kielekroniki kupitia tovuti ya TMX ( https://www.tmx.co.tz/).
Ndugu Waandishi wa Habari, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kupitia Sheria ya Stakabadhi za Ghala Sura ya 339 R.E 2016, imepewa mamlaka ya kutoa leseni kwa Waendesha Ghala kusimamia Ghala Kuu katika ukusanyaji wa bidhaa mbalimbali (mazao ya kilimo na yasiyo ya kilimo). Kwa kuzingatia Kanuni ya 15(2) ya Stakabadhi za Ghala Mwendesha Ghala na Ghala hupatikana baada ya kukidhi vigezo ikiwemo uwezo wa kampuni kusimamia biashara, uwepo wa wataalam wa kusimamia ghalani, kinga na bima za utendaji na uwepo wa uthibitisho wa umiliki au upangishwaji ghala wenye sifa ikiwemo za miundombinu muhimu kama vile mizani mikubwa, jengo imara, ufikaji kiurahisi na mawasilino ya kimtandao.
Ndugu Waandishi wa Habari, Bidhaa hukusanywa kutoka kwa Waweka Mali (wazalishaji, wakulima, wasindikaji n.k) ambao hufikisha ghalani kwa utaratibu uliopo kma vile kupitia Vyama vya Msingi (AMCOS), Vikundi, mtu binafsi au taasisi. Mweka Mali akiashaandikiwa Stakabadhi huweza kutimumia kwa mambo mbalimbali ikiwemo kuuza kwa minada kupitia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), kupata mikopo kupitia mabenki, kuwezesha usindikaji mazao, kuuza kwa minada ya baadae au kutimia kama sehemu salama ya kuhifadhi.
Ndugu Waandishi wa Habari, Kwa matumizi ya Stakabadhi za Ghala kwa ajili ya minada kupitia Soko la Bidhaa (TMX), baada ya bidhaa kukusanywa, Mweka Mali huandikiwa Stakabadhi ya Ghala inayokuwa na taarifa za uzito, idadi, vifungashio na ubora wa bidhaa husika. Taarifa za Stakabadhi za Waweka Mali mbalimbali hujuimishwa pamoja katika Kanzidata ya Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), ambazo hutumiwa kuandaa Katalogi ya Mauzo kisha kunadiwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).
Ndugu Waandishi wa Habari, Soko la Bidhaa Tanzania likishakamilisha minada, mnunuzi hufanya malipo yote kupitia mifumo ya kibenki na kupatiwa nyaraka za kutoa mzigo ghalani. Katika utoaji mnunuzi atatakiwa kujiridhisha ubora wake kabla ya kutoa mazao ghalani. Mzigo ukishapokelewa na mnunuzi, mnunuzi huwajibuka na ubora na usalama wa mzigo hadi anakoufikisha kwa matumizi yake.
Ndugu Waandishi wa Habari, Ukusanyaji wa bidhaa huzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali iliyopo ili kuhakikisha kuwa sifa za bidhaa zinazofikishwa ghalani zinakidhi matakwa ya soko la nje na ndani ili kumuongezea mnunuzi uhakika wa bidhaa anayonunua. Vigezo vya msingi ambavyo hutazamwa ni pamoja na sifa za kifikizia na kikemia za bidhaa kama vile umbile/muundo, unyevu, usafi, hali bidhaa. Aidha, bidhaa hutakiwa kufungashwa kwenye vifungashio vipya na vyenye uzito, idadi na sifa kama zilivyoanishwa katika Viwango Vya Ubora vinavyotolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Ndugu Waandishi wa Habari, Mfumo huu wa stakabadhi za ghala kwa Wanaushirika unatimiza dhana nzima ya Ushirika ambayo ni kuunganisha nguvu ya pamoja kwa lengo la kuwa na nguvu ya soko. Kama mnavyojua, wakulima wetu wengi wao ni wakulima wadogo wadogo na inakuwa ni rahisi sana kulanguliwa kwa kuwa wanakuwa wanazalisha kidogo, lakini kwa kutumia mfumo huu, wanaweza kukusanya mazao yao kwa pamoja kupitia vyama vyao vya Ushirika na kuuza mazao yao na hatimaye kuwa na nguvu ya soko (bargaining power).
Ndugu Waandishi wa Habari, Mfumo wa stakabadhi za ghala unawezesha Soko la bidhaa Tanzania kusaidia wakulima kupitia vyama vya Ushirika kuuza mazao yao kwenye soko lenye ushindani ambapo soko la bidhaa linafanya minada ya wazi kwa njia ya elektroniki. Minada ambayo itakuwa inafanyika kila wiki, inawapa fursa wanunuzi mbali mbali ndani na nje ya nchi kuweza kushiriki na hatimaye kupata bei shindani kutokana na kuwashindanisha wanunuzi hao.
Ndugu Waandishi wa Habari, Mwisho napenda kuwashukuru sana wote mliyoshiriki nasi katika halfa hii, ni mategemeo yetu kuwa taarifa hizi zitawafikia wadau wote wa mazao haya kupitia vyombo vyenu kwa lengo la kutoa uelewa na uhamasishaji kwa ujumla kuhusu matumizi ya mfumo huu.
____________________
Dkt. Benson O. Ndiege
Mrajis wa Vyama vya Ushirika Nchini
Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania
____________________
Godfrey Malekano
Afisa Mtendaji Mkuu
Soko la Bidhaa Tanzania
____________________
Asangye N. Bangu
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala