Mrajis wa Vyama vya Ushirika katika kufanya maboresho ya Daftari la Vyama vya Ushirika amefanya uchambuzi na kuainisha vyama ambavyo havitekelezi majukumu yake ya msingi kwa mujibu wa sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013.
Kwa kuzingatia kifungu 100 cha Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya Mwaka 2013 na kanuni ya 26 ya Kanuni za Vyama vya Ushirika za mwaka 2015, Mrajis ametoa kusudio la kuvifuta vyama vya ushirika 3,436 ambavyo havitekelezi majukumu yake ya msingi na ambavyo havipatikani/havijulikani mahali vilipo.
Kusudio la kufuta vyama vya ushirika 3,436 limetangazwa kwenye Gazeti la Serikali la tarehe 17/01/2020 kupitia Taarifa ya Kawaida (GN No. 54).
Kusudio hilo litadumu kwa muda wa siku 90 tangu lilipotangazwa kwenye Gazeti la Serikali ambapo ndani ya kipindi hicho, chama chochote chenye pingamizi kuhusiana na kusudio la kufutwa kinaweza kuwasilisha kwa maandishi utetezi wake kwa Mrajis wa Vyama Vya Ushirika kupitia Ofisi za Warajis Wasaidizi wa Mikoa. Baada ya kipindi hicho kwisha ndipo vyama hivyo vitafutwa na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali.