SERIKALI haitaingilia Vyama vya Ushirika nchini vinavyofuata sheria na taratibu katika uendeshaji wake, isipokuwa pale panapojitokeza ukiukwaji wa Misingi ya Ushirika na panapokuwa na ubadhilifu wa mali za Wanaushirika unaofanywa na baadhi ya viongozi wa vyama hivyo.
Angalizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Titus Kamani pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, leo Alhamis, Desemba 19, 2019 mjini Tabora, walipokuwa wakiongea kwenye Kikao cha Wadau wa Ushirika mkoa wa Tabora kilichofanyika katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi – Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
“Serikali haiwezi kuingilia Vyama vya Ushirika vinavyofuata sheria na taratibu katika uendeshaji wake isipokuwa panapojitokeza ukiukwaji wa Misingi ya Ushirika na panapokuwa na ubadhilifu na wizi wa mali za Wanaushirika unaofanywa na baadhi ya viongozi, hatutanyamaza, tutachukua hatua,” amesema Dkt. Kamani.
Dkt. Kamani amewahimiza Viongozi wa Vyama vya Ushirika kuwa waaminifu na waadilifu katika kusimamia mali za wanaushirika walizokabidhiwa na wanachama wenzao kuzisimamia kwa niaba yao na kuweza kupata faida ya pamoja itayowawezesha kuboresha maisha yao.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Aggrey Mwanri, amesema Serikali mkoani humo haitasita kuwachulia hatua kali za kisheria viongozi wa vyama vya ushirika wanaokiuka sheria na taratibu za uendeshaji wa vyama ushirika kwa kisingizio kuwa ushirika ni mali yao na Serikali haiwezi kuwaingilia.
“Ushirika siyo kichaka cha baadhi ya watu kuiba; hatutaruhusu, tutawakamata wakati wanaiba, hatutasubiri na tutawatia ndani. Wapo viongozi wa ushirika wazuri tu, anaweza kuwa Mwenyekiti au Katibu Meneja, hao watakuwa marafiki wa Serikali na hawatasumbuliwa,” amesema Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Akizungumza katika Kikao hicho, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tabora ambaye ni pia ni Mwanaushirika, Hassan Wakasuvi, amewataka viongozi wa vyama vya ushirika katika maeneo yanayolima zao la Tumbaku wasimamie masharti wanayojiwekea ili kuondokana na adha inayojitokeza wakati msimu wa kuuza Tumbaku.
“Viongozi wa vyama vya ushirika simamieni masharti mnayojiwekea, ili kuinua thamani ya zao la Tumbaku na kuondokana na bei za aina mbili, ikiwemo bei ya makinikia ambayo inakuwa ni ya kinyonyaji kwa wakulima,” amesema Wakasuvi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, akizungumza katika Kikao hicho, amewataka Wanaushirika kote nchini kuchangamkia Bima ya Afya inayotolewa mahsusi kwa wanachama wa Vyama vya Ushirika – Ushika Afya.
“Viongozi wa Vyama vya Ushirika wahimizeni Wanachama wenu kujiunga na Bima ya Afya inayotolewa kwa wanachama wa Vyama vya Ushirika – Ushika Afya, kwa kuwa ni muhimu kwa afya na maendeleo ya familia zao; na inatolewa kwa gharama nafuu ya Shilingi 76,800/ (mtu mzima) na Shilingi 50,400/ (mtoto) kwa mwaka,” amesema Mhe. Ummy Mwalimu.