Serikali ina mkakati wa kuendeleza na kuimarisha Ushirika kwa kuanzisha na kufufua viwanda ili kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa Wanaushirika, ambapo Serikali imedhamiria kuona kwamba Vyama vya Ushirika vinashiriki katika ujenzi wa Viwanda nchini; ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano kuanzia Mwaka 2016 - 2020.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji, Mhe. Anjella Kairuki katika maadhimisho ya maonesho ya Kilimo na sherehe za Wakulima Nanenane Kitaifa leo tarehe 03/08/2020 kwenye Viwanja vya Nyakabindi Simiyu.
Waziri Kairuki akimwakilisha Waziri Mkuu katika Siku Maalum ya kuhamasisha Ushirika katika maonesho hayo amesema Serikali imedhamiria kuendeleza Ushirika nchini ikiwa ni Sera ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali tangu Uhuru hadi sasa, ambapo Ilani ya CCM yam waka 2015-2020 imeainisha kuwa Ushirika ni muhimili mkuu wa ujenzi wa Uchumi imara na ustawi wa Jamii ya Watanzania.
“Katika kutekeleza dhamira hii tumeshuhudia Vyama vya Ushirika vikianzisha na kufufua viwanda 75 katika maeneo mbalimbali hapa nchini katika kipindi cha mwaka 2018/2019 kwaajili ya kuchakata mafuta ya Alizeti na Chikichi, kutengeneza samani za nyumbani, kuchakata pamba na mazao ya nafaka pamoja na usindikaji wa maziwa, Idadi hiyo inafanya viwanda vinavyomilikiwa na Vyama vya Ushirika kuongezeka kutoka viwanda 133 mwaka 2018 hadi kufikia viwanda 208 mwaka 2019,” alisema Waziri Kairuki
Akimkaribisha Waziri Kairuki kuongea na Wanaushirika na Wananchi kwa ujumla, Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga amesema Vyama vya Ushirika vimekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma bora na kuleta ustawi wa Maendeleo ya Taifa, ambapo Wanachama wa Vyama vya Ushirika wamepata manufaa mbalimbali ya kuwemo kwenye ushirika.
“Ushirika umeweza kuwapatia wakulima bei nzuri ya mazao yao, kuimarisha kipato chao na kuwawezesha kununua vyombo vya usafiri, kujenga nyumba bora na kuwasomesha watoto wao katika ngazi mbalimbali za elimu na wengine wamefikia hadi elimu ya Chuo Kikuu na wengine wameweza kugharimia matibabu ya familia zao,” alisema Waziri Hasunga.
Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) vimeendelea kutoa huduma za fedha kwa wanachama wake ambapo thamani ya mikopo iliyotolewa imeongezeka kutoka Shillingi Trillioni 1.3 Desemba, 2018 na kufikia Shillingi Trillioni 1.5 Desemba 2019 sawa na ongezeko la asilimia 15. Vilevile jumla ya thamani ya Hisa, Akiba na Amana imeongezeka kutoka Shillingi Billioni 654 Desemba 2018 na kufikia Shillingi Billioni 819 Desemba, 2019 sawa na ongezeko la asilimia 25.
Akizungumza katika hafla hiyo Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege amesema Ushirika umemwezesha mkulima kupata soko la mazao yao kupitia ushirika kwa kushirikiana na wadau kama Soko la Bidhaa (TMX) na Bodi za Mazao. Mazao yaliyouzwa kwa mwaka 2020 ni pamoja na Ufuta, Choroko, Dengu, Mkonge, Pamba yenye thamani ya Shillingi Trillioni 2.7.
Katika hafla hiyo Waziri Kairuki alizindua Program mbalimbali za kuimarisha na kuendeleza Ushirika Programu ya Uhamasishaji wa SAFI, Programu ya kusaidia vyama vya Ushirika kupitia Shirika lisilo la Kiserikali la AGRITERRA na kukabidhi mbolea kwa vyama vya Ushirika vilivyoagiza kwa mfumo wa pamoja kupitia TFRA na kutoa tuzo kwa Wadau waliowezesha Vyama vya Ushirika.