Serikali kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Vyama vya Ushirika, Namba 6 ya mwaka 2013, kifungu cha 100 na kanuni ya 26, inakusudia kufuta Vyama vya Ushirika 3,436 ambavyo havitekelezi majukumu yake ya msingi na havipatikani au havijulikani vilipo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, leo Januari 05, 2020 Jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga, amemwagiza Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, kutoa Notisi kwenye Gazeti la Serikali ya muda wa siku 90 ya kusudio la kutaka kufuta vyama vya ushirika ambavyo havitekelezi majukumu yake ya msingi.
“Ninamuagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika kutangaza mara moja kusudio la kufuta vyama 3,436 ambavyo havitekelezi majukumu yake ya msingi na havipatikani/havijulikani vilipo. Vyama hivi vimetapakaa kwenye Mikoa yote Tanzania Bara,” amesema Mhe. Hasunga.
Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika kifungu cha 100, chama kinaweza kikafutwa kwa sababu mbali mbali ikiwa ni pamoja na: kutokuwa na ofisi tangu kiandikishwe; havijulikani vilipo na viongozi wake hawafahamiki na hawapatikani; kushindwa kutekeleza takwa la kisheria la kutayarisha makisio ya mapato na matumizi na kuyapeleka kwa mrajisi kuyapitisha; kushindwa kutayarisha taarifa ya mwaka, kushindwa kufunga mahesabu na kuyapeleka COASCO kwa ukaguzi, kutofanya mikutano ya mwaka ya wanachama wote na bodi zao, Chama kushindwa kufanya shughuli zake ndani ya miezi sita tangu kiandikishwe; Idadi ya wanachama kupungua kwa mujibu wa mahitaji ya kisheria.
Asilimia kubwa ya vyama vya ushirika vilinavyokusudiwa kufutwa ni Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) ambavyo ni asilimia 73.8, vyama hivi vingi ni matokeo ya Mfuko wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Mfuko huu ulilenga katika kuwawezesha wananchi kiuchumi ambapo wananchi walio wengi walianzisha SACCOS kwa lengo la kupata mikopo kutoka kwenye mfuko huo. Aidha, vyama ambavyo havikupata mkopo havikuendelea na majukumu yake na hata vilivyopata mikopo baada ya kupata mikopo walitelekeza vyama vyao jambo ambalo lilipelekea kuwa na SACCOS nyingi ambazo hazifanyi kazi.
Vyama vya Ushirika ambavyo havifanyi kazi vizuri vimetajwa kwa mchanganuo ufuatao SACCOS (2,537), AMCOS (264), Mifugo (82), Vyama vya walaji (25), Vyama vya huduma (72), Vyama vya ufugaji nyuki (17), nyumba (8), madini (23), Viwanda (102), uvuvi (37), umwagiliaji (31), vyama vikuu (3), na vinginevyo (235).
Idadi ya vyama vya Ushirika kimkoa vinavyokusudiwa kufutwa ni kama ifuatavyo: Mwanza (393), Pwani (335), Kagera (301), Morogoro (298), Arusha (282), Tabora (282), Kigoma (207), Mara (151), Tanga (136), Geita (119), Manyara (116), Iringa (92), Lindi (85, Mbeya (78), Rukwa (70), Dodoma (68), Singida (59), Songwe (54), Mtwara (52), Kilimanjaro (49), Njombe (40), Simiyu (40), Dar es salaam (39), Ruvuma (39), Shinyanga (34) na Katavi (17).
Mpaka sasa Daftari la Mrajis wa Vyama vya Ushirika lina jumla ya vyama 11,149 vilivyoandikishwa. Kati ya Vyama hivyo, 3,436 havijulikani vilipo (hewa), vyama 1,250 vimesinzia na vyama 6,463 vipo hai.