Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) imeongeza udhibiti na usimamizi wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kwa kuhakikisha Vyama vyote vinajisajiliwa kwa kutumia mifumo ya TEHAMA inayopatikana kupitia Tovuti ya Tume www.ushirika.go.tz
Hayo yamesemwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege Jumatano Juni 23, 2020 wakati wa uzinduzi wa mfumo wa TEHAMA wa kuomba na kutoa leseni kwa njia ya mtandao pamoja na kujadili mikakati pamoja na mipango ya Tume katika kusimamia na kusimamia katika utendaji kazi na utoaji huduma kwa wanachama na wananchi ili kutoa muelekeo mpya wa utendaji wa SACCOS nchini. Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi pamoja na watendaji wa Vyama vya SACCOS kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Mrajis alieleza kuwa lengo la Tume kuanzisha mfumo huo ni kusaidia kuondokana na changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikijitokeza katika usajili wa Vyama pamoja na gharama kwa waombaji wa leseni kusafiri umbali mrefu kupeleka nyaraka pamoja na taarifa zinazotakiwa kwaajili ya kuomba leseni husika.
Wataalamu wa Tume watakuwepo kuwapa ufafanuzi hatua kwa hatua namna mfumo huu utakavyofanya, mfumo huu utatusaidia wote Vyama pamoja na Tume kama msimamizi katika Sekta ya Ushirika. Mfumo huu utasaidia kuvitambua vyama kwa urahisi kwa kutunza taarifa sahihi wakati wote, kuvisajili na utoaji wa ripoti,” alisema Mrajis
Katika hotuba ya Mrajis alisema Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango iliandaa Sera ya Huduma Ndogo za Fedha yam waka 2017. Katika utekelezaji wa azma hiyo, Serikali ilitunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha yam waka 2018, ambapo Benki Kuu ya Tanzania yenye jukumu la kusimamia taasisi zinazotoa Huduma Ndogo za Fedha ilikasimisha Mamlaka na majukumu yake kwa TCDC tarehe 22 Nov 2019 kupitia Gazeti la Serikali lenye GN.887.
Aliongeza kwa kuwakumbusha wajumbe kuwa Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha zilizoanza kufanya kazi tarehe 01 Nov 2019.
“Muda wa mpito uliotolewa kwenye Sheria ni mwaka mmoja yaani kuanzia 01 Nov 2019 hadi 31 Oktoba 2020. Hivyo, SACCOS zote zinapaswa kuwa zimeombwa na kupewa leseni,” alisisitiza Dkt. Ndiege
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tanesco SACCOS Thomas Samo ameishukuru Tume kwa niaba ya washiriki wa kikao hicho cha uzinduzi kwa kuendeleakuwa bega kwa bega katika kuhakikisha Sekta ya Ushirika inaendelea kuimarika. Vilevile alitumia fursa hiyo kuzitaka SACCOS nchini kuitikia wito wa kusajili haraka na kupata leseni za usimamizi kama ilivyoelekezwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Sheria Huduma Ndogo za Fedha. Akiongeza kuwa kufanya hivyo licha ya kufuata matakwa ya Kisheria pia itasaidia kuimarisha uendeshaji na utendaji wa SACCOS kutokana na uwezo wa mifumo kutunza taarifa kwa usahihi wakati wote zitakapohitajika, jambo ambalo litaongeza tija na ufanisi kwa Vyama na Sekta ya Ushirika kwa ujumla.