Tume ya Maendeleo Ushirika Tanzania (TCDC) imekutana katika Kikao cha Pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa lengo la kuimarisha usimamizi na maendeleo ya Vyama vya Ushirika nchini.
Kikao hicho kimefanyika leo Julai 15, 2020 Jijijini Dodoma katika makao makuu ya Tume ya Maendeleo Ushirika Tanzania, ambapo ujumbe wa TAKUKURU uliongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Brigedia Jenerali John Mbungo, na ujumbe wa TCDC uliongozwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtedaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege.
Kikao hicho kililenga kuainisha majukumu ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) na majukumu ya TAKUKURU ili kuwa na uelewa wa pamoja katika kuimarisha usimamizi na maendeleo ya Vyama vya Ushirika nchini.
TAKUKURU iliwasilisha Taarifa ya Uchunguzi na Fedha zilizokusanywa na Taasisi hiyo kwa niaba ya Vyama vya Ushirika nchi nzima baada ya kukabidhiwa kazi hiyo na Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga.
Wajumbe wa Kikao hicho vilevile walijadili mfumo na utaratibu unaotumiwa na TAKUKURU katika urejeshaji wa fedha zilizokusanywa kwenye Vyama vya Ushirika na kuangalia njia na mbinu za kuzuia mianya ya wizi na ubadhirifu katika Vyama vya Ushirika. Aidha, TAKUKURU na TCDC walikubaliana kuhusu maeneo ya kushirikiana kati ya taasisi hizo mbili.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo, amepongeza ushirikiano uliotolewa na Tume ya Maendeleo Ushirika kwa TAKUKURU wakati wakitekeleza maagizo ya viongozi Serikali katika urejeshaji wa fedha kwenye Vyama vya Ushirika zilizokuwa zimechukuliwa bila kufuata utaratibu.
“Tuleteeni matatizo na changamoto zinazohusu ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya watu wanaoviibia Vyama vya Ushirika ili tushughulike nao na kuhakisha kuwa mali za wanaushirika zinakuwa salama,” amesema Brigedia Jenerali Mbungo.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege amesema kuwa kazi iliyofanywa na TAKUKURU katika katika urejeshaji wa fedha kwenye Vyama vya Ushirika zilizokuwa zimechukuliwa bila kufuata utaratibu imewezesha kutoa ujumbe mahsusi kuwa fedha na mali za Wanaushirika hazitakiwi kuchezewa.
“Tutaendelea kushirikiana na TAKUKURU katika kuhakikisha kuwa mali za wanachama wa Vyama vya Ushirika zinalindwa na kuwanufaisha Wananchi; na Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa Mikoa na Maafisa Ushirika wa Wilaya waendelee kushirikiana na Maafisa wa TAKUKURU katika maeneo yao ili kulinda mali za Wanaushirika,” amesema Dkt. Ndiege.