Wanaushirika wametakiwa kuchukua hatua dhidi ya uharibifu wa mazingira nchini ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na uendelevu wa shughuli mbalimbali za kiuchumi katika Vyama vya Ushirika.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya katika maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika leo Jumatatu Juni 6, 2020 Mkoani Morogoro. Maadhimisho ambayo ni ya 19 kuadhimishwa hapa nchini yaliyokuwa na kauli mbiu Ushirika kwa mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.
Akifafanua kuhusu Kauli Mbiu hiyo Katibu Mkuu amesema ni wajibu wa Wanaushirika kuhakikisha kuwa wanafuata kanuni na mbinu bora za utunzaji wa mazingira ili kuwa na uendelevu wa shughuli wanazofanya katika Vyama. Akitaja baadhi ya mbinu hizo kama vile upandaji miti, kilimo mseto, kilimo cha umwagiliaji na jitihada nyingine nyingi
“Ili tufanikiwe ni lazima tuendane na mbinu bora za utunzaji wa mazingira, kwani wanaushirika wote kwa namna moja au nyingine tunaathirika pale mazingira yanapokuwa sio rafiki”, alisema Katibu Mkuu
Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akiongea na wanaushirika katika maadhimisho hayo alitoa wito kwa Vyama vya Ushirika kuhakikisha kuwa wanafanyakazi kuhakikisha kuwa wanaushirika wananufaika na shughuli za zinazofanywa na Vyama hivyo hususani mali za Ushirika. Mrajis aliongeza kuwa ni muhimu kwa mwanachama mmoja mmoja apate manufaa na chama
“Ni wakati sasa kwa Vyama vya Ushirika kuhakikisha kuwa wanawajibika kwa Wanaushirika, Vyama hakikisheni mnafanya kazi kwa maslahi ya Wanachama wa Ushirika na wanachama wengi zaidi wanufaike na vyama vyao vya Ushirika,” alisema Dkt. Ndiege
Nae Mshauri wa Kibiashara wa Shirika lisilo la Kiserikali (NGO) la Agriterra linalojishughulisha na masuala ya Ushirika nchini Bw. Waziri Mikidadi Agriterra akisoma hotuba yake kwa wanaushirika alieleza kuwa Shirika hilo Programu ya kusaidia vyama vya Ushirika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi 3 ikiwemo Uganda, Kenya na Tanzania. Akielezea manufaa ya hiyo alifafanua kuwa program hiyo itaongeza uzalishaji na kukuza kipato kwa wakulima wadogo wasiopungua 300,000.
Aidha, Programu hiyo ilielezwa kuwa itaimarisha biashara kwa makampuni madogo 50 na vyama vya ushirika 30 kati ya hivyo 25% vinaongozwa na wakinamama na vijana.
Akitoa salamu kwa niaba ya Wanaushirika ambaye pia Mjumbe wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo SCCULT (1992) Ltd Mwl. Anna Lupiano ameshauri elimu ya Ushirika itolewe kuanzia ngazi ya familia, mashuleni, vyuoni. Akaongeza kwa kuwasisitiza wanaushirika kuendelea kuboresha mazingira kwa kupanda miti katika mazingira na maeneo ya vyama vya Ushirika.