Vyama vya Ushirika wa mazao vimetakiwa kuchakata mazao yanayozalishwa na wakulima kwa kuongeza mnyororo wa thamani kupitia viwanda vya Ushirika ili kumnufaisha mkulima kwa kumwezesha kupata bei nzuri ya mazao yake na kuongeza ajira.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya, jana Mei 7, 2020 alipozungumza na Makamishna wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) na Menejimenti ya Tume Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuongeza juhudi za kufufua viwanda vya Ushirika kwa lengo la kuongeza mapato ya Vyama vya Ushirika na kumnufaisha mkulima. Aidha, Vyama vya Ushirika vimetakiwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuanzisha na kuendeleza Viwanda nchini.
“Tutafute mbinu za kuongeza tija katika mazao ya wakulima wetu ili wasiendelee kuuza mazao ghafi, hii itakuwa ni namna bora ya kuimarisha, kurejesha ushirika imara na kuongeza imani ya wanaushirika,” alisema Katibu Mkuu
Bwana Kusaya amesema moja ya changamoto zinazowakabili wakulima mara kwa mara wakati wa mavuno ni upatikanaji wa vifungashio hususan magunia. Hivyo, alisema changamoto hiyo igeuzwe kuwa fursa kwa kuangalia namna bora ya uchakataji wa zao la katani kwa lengo la kupata vifungashio kwa urahisi na bei nafuu kwa wakulima.
Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo amesema mahitaji ya mbolea kwa wakulima ni makubwa, hivyo itumike kama fursa nyingine kwa Vyama vya Ushirika kuanzisha viwanda vya mbolea, jambo ambalo litampa mkulima nafuu ya gharama za kilimo.
Bwana Kusaya ameitaka Tume kuendelea kuhamasisha kilimo cha mazao ya kimkakati kama vile Pamba, Tumbaku, Kahawa, Chai na Korosho ili kuongeza malighafi zinazohitajika kwaajili ya viwanda.
“Tuendelee kuhimiza wananchi na wakulima wetu kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara ambayo yanahitajika kwaajili ya malighafi katika viwanda vyetu vya ndani na kwenye masoko ya nje ili kulipatia Taifa fedha za kigeni,” amesema Bwana Kusaya.
Akizungumza kwa niaba ya Makamishna wenzake, Kamishna Abdul Marombwa, alimshukuru Katibu Mkuu kwa maelekezo na ushauri alioutoa kwa kuwa unaenda kuongeza tija na kasi ya ukuaji wa Sekta ya Ushirika na kuahidi kuwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wa Sekta ya Ushirika ili kuhakikisha wanaushirika na Taifa linapata manufaa kupitia Sekta ya Ushirika.