Wakulima wa Vyama vya Ushirika nchini wamepewa wito wa kuboresha maisha yao kwa kuweka akiba baada ya msimu wa mavuno ya mazao yao ili akiba hizo ziwasaidie hususan wanapopata changamoto mbalimbali za kimaisha.
Wito huo umetolewa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) Dkt. Benson Ndiege wakati alipotembelea Chama cha Ushirika wa Wakulima wadogo wadogo wa Kilimo cha umwagiliaji Mpunga Dakawa (UWAWAKUDA LTD) kwenye ziara ya Kikazi, Mkoani Morogoro hivi karibuni.
Mrajis amesema kuwa wanachama wa Ushirika wanaweza kutumia fursa ya kuwa pamoja katika Chama kwa kuimarisha Ushirika wao kwa kujiwekea utaratibu maalum wa kutunza akiba zinazotokana na mauzo ya mazao pale wanapovuna. Alibainisha kuwa utaratibu huo utakaposimamiwa vizuri kwa taratibu za kiushirika unaweza kuongeza fursa nyingine ya kuwa na Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) inayotokana na wanachama wa UWAWAKUDA.
“Kila mkulima anapovuna anaweza kujiwekea Akiba katika Mfuko wao ambao utatumiwa na Wanaushirika kwa mahitaji yao mbalimbali pamoja na dharura zinapojitokeza kwa mwanachama,” alisema Mrajis
Aidha, Akielezea Chama hicho Mwenyekiti wa UWAWAKUDA Bw. Thomas Kalema alisema kuwa Chama hicho cha Ushirika chenye jumla ya Eka 5,000 za umwagiliaji kilianzishwa rasmi tarehe 24 Julai 2006 kina Jumla ya Wanachama 935 ambao kati ya hao 552 ni wanaume, 376 ni wanawake pamoja taasisi za kidini 7. Alibainisha kuwa Mradi huo umekuwa ukipata ufadhili kutoka Serikalini pamoja na wadau wengine wa maendeleo kwa lengo la kuwakomboa wananchi kiuchumi.
Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bertha Chilosa alipata fursa ya kueleza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa Ushirika miaka ya 2004 kurudi nyuma, hali ya maisha ya wakazi wa Dakawa ilikuwa duni sana ukilinanisha na baada ya Ushirika kuanzishwa. Alibainisha baadhi ya manufaa yaliyopatikana na mradi huo ni pamoja na Wanachama wengi kuweza kujenga nyumba bora za kisasa, fursa za mikopo kwenye taasisi za kifedha, huduma kwa jamii, upatikanaji wa ajira akitoa mfano kuwa zaidi ya vibarua 5,000 kutoka Dakawa na maeneo jirani katika kipindi cha msimu wa kilimo. Aliongeza kuwa vijana wengi kupitia shamba la UWAWAKUDA wamefungua biashara mbalimbali zinazowasaidia kuhudumia familia na kuchangia pato la Taifa.