Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini, Dkt. Titus Kamani ametoa siku kumi na nne (14) kwa watu waliochukua mali na fedha za vyama vya ushirika kuzirejesha katika vyama hivyo la sivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Dkt. Kamani ametoa agizo hilo mkoani Dodoma jana Februari 01, 2018 wakati akizungumza na wafanyakazi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (makao makuu) na kusema kuwa ni aibu kwa vyama vikuu kushindwa kujiendesha kutokana na ubadhirifu unaofanywa na viongozi wa vyama hivyo.
“Lazima mali hizo zirudi, hata kama waliochukua walishaondoka kwenye madaraka, kama wako Tanzania hii na wako hai, lazima warudishe mali za wanachama; tutawafuatilia mahali popote walipo. Ni aibu chama kikuu kinachomiliki mamilioni ya fedha kushindwa kujiendesha,” anasema Dkt. Kamani.
Dkt. Kamani amewataka Watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kufanya kazi kwa weledi na kujituma ili kusimamia mali za Wanaushirika na kuongeza kasi ya uhamasishaji wa uanzishwaji wa vyama vya ushirika na kuhakikisha kuwa vinakuwa endelevu na kuwainua wananchi wengi zaidi kiuchumi na kijamii.
Akimkaribisha Mwenyekiti kuzungumza na Watumishi wa Tume – Makao Makuu, Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Charles Malunde alisema kuwa Watumishi wameanza kufanya maboresho katika sekta ya ushirika na wanaamini kuteuliwa na kuanza kazi kwa Mwenyekiti na Makamishna wa Tume kutaongeza nguvu na kasi ya kuwahudumia Wanaushirika.
“Kumekuwa na mwelekeo mwingine kwenye ushirika na watu wamekata tamaa wakisikia neno ushirika, lakini kwetu sisi bado tuna ujasili wa kusema kwamba sehemu pekee ya kuwalinda wakulima na watu wenye kipato cha chini wasinyonywe ni kupitia vyama vya ushirika,” anasema Naibu Mrajis.
Aidha, pamoja na kukutana na Watumishi wa Tume jana, Makamishna vilevile walitembelea Vyama vya ushirika vya Arusha Road SACCOS na Mpunguzi AMCOS.