Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amewataka Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa mikoa kutokufanya kazi za utendaji katika vyama vya ushirika badala yake wafanye kazi ya wasimamizi wa vyama hivyo.
Akizungumza kwenye Kikao kazi cha Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa Mikoa na Viongozi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania kilichofanyika leo tarehe 13 Januari, 2020 Jijini Dodoma, Dkt. Ndiege amesema kuwa baadhi ya Watumishi katika Sekta ya Ushirika wakiwemo baadhi ya Warajis Wasaidizi wamekuwa wakijiingiza kwenye utendaji wa vyama na kushindwa kutekeleza majukumu yao.
“Kuweni Waadilifu, sisi kama Tume ni wasimamizi wa vyama, siyo watendaji katika vyama. Kuna maeneo mengine Warajis mnajiingiza kwenye utendaji wa vyama, acheni kuwa watendaji wa vyama kwa kuwa mnashindwa kutekeleza majukumu yenu na kujikuta mnajiingiza kwenye ubadhirifu,” amesema Dkt. Ndiege.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika amesema kuwa Tume imekuwa ikichukua hatua kwa Watumishi walioko chini yake wanaothibitika wameenda kinyume na taratibu na amewataka Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa Mikoa kusimamia utaratibu uliowekwa kisheria.
Aidha, Dkt. Ndiege amewataka Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa Mikoa kushirikiana kwa karibu na ofisi nyingine za serikali katika kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuongeza mahusiano na Taasisi nyingine (Wadau wa Ushirika) zinazofanya kazi na Vyama vya Ushirika.
“Mkiwa na mahusiano mazuri na Halmashauri, mtaweza kuwatumia Maafisa Ushirika walioko chini ya Wakurugenzi kwa kuwa wote ni watumishi wa Serikali na mnahudumia vyama vya ushirika. Kinachotakiwa ni mahusiano mazuri ya kiutendaji ikiwa ni pamoja na matokeo chanya ya usimamizi wa Vyama vya Ushirika,” amesema Dkt. Ndiege.
Katika kuboresha utendaji kazi, Mrajis wa Vyama vya Ushirika ameelekeza kuwa kuanzia sasa vyama vyote vya ushirika vilivyopo katika Mkoa vitasimamiwa na Warajis Wasaidizi wa Mikoa husika.
“Mnatakiwa kusimamia vyama vyote vya Ushirika katika mikoa yenu, hakikisheni kuwa, kila kazi ya usimamizi wa Vyama utakaofanyika katika maeneo yenu lazima taarifa ya kazi itolewe makao makuu, si kwamba mnapewa mamlaka ya kutawala bila kutoa taarifa kwa mamlaka za juu,” amesema Dkt. Ndiege