Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga, amemwagiza Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege kufanya tathmini ya utendaji kazi wa Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa Mikoa na Watendaji wa Tume kwa ujumla ili kufanya mabadiliko muhimu kwa lengo la kuongeza ufanisi katika usimamizi wa Vyama vya Ushirika.
Akizungumza na Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa Mikoa na Viongozi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania leo tarehe 15 Januari, 2020 Jijini Dodoma, Mheshimiwa Hasunga amesema kuwa changamoto nyingi zinazojitokeza katika Sekta ya Ushirika zinasababishwa na baadhi ya Warajis Wasaidizi kutokusimamia ipasavyo vyama vya ushirika vilivyopo katika maeneo yao.
“Mrajis, fanya tathmini ya Warajis Wasaidizi wa Vyama vya Ushirika wa Mikoa na Watendaji wa Tume kwa ujumla na ikiwezekana fanya mabadiliko muhimu kwa lengo la kuongeza ufanisi katika usimamizi wa Vyama vya Ushirika,” amesema Waziri Hasunga.
Aidha, Waziri Hasunga ameagiza watumishi wa Tume waliopo makao makuu wapunguzwe na kuhamishiwa kwenye ofisi za Tume katika ngazi za mikoa na wilaya ili kuongeza nguvu ya usimamizi wa vyama vya ushirika katika mikoa na wilaya.
Kufuatia maelekezo ya Waziri Hasunga, Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, ameahidi kutekeleza malekezo yaliyotolewa ili kuimarisha utendaji kazi wa Tume kwenye usimamizi wa vyama vya ushirika nchini.