Mrajis Afuta Usajili wa Ushirika Tower Joint Enterprise

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege ametoa maagizo ya kufutwa kwa Usajili wa Chama cha Ushirika cha Ushirika Tower Joint Enterprise pamoja na kuvunja Kamati iliyokuwa ikiratibu uanzishaji wa Benki ya Ushirika ya Kitaifa.

Maagizo hayo ameyatoa leo Ijumaa Desemba 11, 2020 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 25 wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika uliofanyika Jijini Dodoma ambapo ameagiza Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC) kuwasilisha andiko la kuanzisha Benki ya Ushirika ya Kitaifa

Mrajis amefikia uamuzi huo kutokana na dosari nyingi zilizojitokeza kufuatia masuala ya urejeshaji wa mkopo ulichukuliwa na TFC wa majengo pacha yaliyopo Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam; ambapo Chama cha Ushirika Tower Joint Enterprise kimefutwa ili kupisha TFC kusimamia Hisa za Wanachama na umiliki wa moja kwa moja wa majengo hayo bila kupitia mmiliki mwingine kwa lengo la kuongeza uwazi na uwajibikaji.

Dkt. Ndiege alifafanua kuwa TFC ilichukua Mkopo wa Shillingi Billioni 23 kwaajili ya ujenzi wa majengo pacha, na hivi sasa inakadiriwa thamani ya majengo hayo kuwa Shillingi Billioni 53. Hivi sasa deni hilo kwa linakadiriwa kufikia kiasi cha Shillingi Billioni 59.  

“Lazima tufanye kazi kwa maslahi ya Wanachama wetu wa Ushirika hatuwezi kuvumilia mambo yanayofanyika kinyume na hilo hivyo Chama cha Ushirika Tower Joint Enterprise kuanzia sasa kinafutwa ili kuongeza tija kwa Shirikisho la TFC,” alisema Dkt. Ndiege

Aidha, Mrajis ameelekeza TFC kuwasilisha upya andiko la kuanzisha Benki ya Ushirika ya Kitaifa litakaloanzisha Benki kwaajili ya kuhudumia Wanaushirika kitaifa. Katika kikao hicho Mrajis ameivunja Kamati iliyokuwa ikiendesha mchakato huo kutokana na kutoridhishwa na utendaji wake wa kazi kwa kutoleta matokeo tarajiwa tangu 2012.

“Kamati iliyokuwa ikishughulikia suala la uanzishaji wa Benki haina kazi tena kuanzia sasa, fedha na hisa za Wanachama zisiguswe wala kutumika vinginevyo hadi maelekezo mengine yatakapotolewa,” alisisita Dkt. Ndiege

Mrajis aliongeza kuwa TFC inapaswa kuendelea kuweka mipango Mkakati yenye tija kwa lengo la kuvijengea uwezo Vyama vya Ushirika na amehimiza kutolewa kwa elimu ya Ushirika, Bima pamoja na kutafuta ufumbuzi wa changamoto za pamoja za Vyama vya Ushirika. Aidha, amevitaka Vyama vya Ushirika kuendeleza Ushirikiano baina yao kama sehemu ya utekelezaji wa misingi ya Ushirika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TFC Theresia Chitumbi amesema Shirikisho limepokea maagizo kwaajili ya kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Serikali. Amesema Shirikisho hilo litaendelea kuboresha utendaji wake pamoja na kuvijengea uwezo Vyama vya Ushirika.

Aidha, Chitumbi amesema baadhi ya masuala yatakayozingatiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya Uandishi wa Vitabu vya Ushirika, ufungaji sahihi wa mahesabu ya Vyama ili kuvisaidia Vyama kufanya kazi kwa tija zaidi.

Mwisho